Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na tetemeko la ardhi pamoja na tsunami iliyoikumba Indonesia Ijumaa iliyopita imepaa hadi watu 1,200, kwa mujibu wa Wakala wa kudhibiti majanga nchini humo.

Idadi hiyo imeongezeka kwa kasi kutoka watu 844 waliokuwa wametajwa kupoteza maisha. Tetemeko lenye magnitude 7.5 liliishambulia kisiwa cha Sulawesi na kusababisha tsunami iliyopiga pwani ya jiji la Palu.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Indonesia limeeleza kuwa miili ya wanafunzi 34 ambao ni kati ya wanafunzi 86 waliopotea walipokwenda kanisani, imekutwa miongoni mwa waliokufa kwa kufukiwa na mmomonyoko wa udongo. Hata hivyo, wanafunzi wengine 52 bado hawajulikani walipo.

Rais wa nchi hiyo, Joko Widodo alikagua maeneo ambayo yameathiriwa na tetemeko hilo na kuomba msaada wa kimataifa.

“Vituo vya umeme karibu vyote vimehariwa. Ni viwili pekee kati ya vituo saba ndivyo vinavyofanya kazi na kusambaza mafuta,” alisema.

Aliongeza kuwa jitihada za uokoaji zinaendelea kufanyika pamoja na kutatua changamoto ya kutokuwepo barabara katika maeneo mengi baada ya kuharibiwa na tetemeko.

Simba SC yawapongeza na kuwaondoa hofu mashabiki
McGregor aahidi kumpasua Khabib Jumamosi hii