Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwasimamisha kazi Maafisa watatu wa shirika hilo kupisha uchunguzi kwa kufanya unyang’anyi na kuomba rushwa ya shilingi milioni 100 katika kiwanda cha Smart Industries Limited kilichopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam walichokwenda kukifanyia ukaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Naibu Waziri Kigahe amesema kuwa maafisa hao walienda kufanya ukaguzi kinyume na majukumu ya ofisi na kufanya ukaguzi usiotambulika na ofisi ambapo amewataja watumishi hao kuwa ni Suleiman Ally Banza Afisa Viwango TBS, Issa Mbaruk ambaye ni Dereva na Thomas Elisha Afisa usafirishaji.
“Mtumishi mmoja wa TBS ambaye anaitwa Suleimani Banza alienda katika kiwanda cha Smart industries Limited kilichopo maeneo ya Kijitonyama akiwa na lengo la kukagua bidhaa ambazo zimepitwa na muda lakini kutokana na kazi zake yeye si mkaguzi bali ni mtu wa kuweka viwango hivyo aliingilia jukumu sio la kwake,” amesema Kigahe.
Aidha, Kigahe ameliomba Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU kuwachukua watumishi hao na kuwafanyia uchunguzi ili kujua mlolongo mzima wa uhujumu na kuchukua hatua kali za kisheria.
Kigahe ameiasa TBS kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi hao kulingana na taratibu na sheria za utumishi wa umma, na kuwaasa wafanyakazi wote wa TBS kufanya kazi kwa bidii na kuwa waadilifu.