Maafisa Viungo wa Halmashauri zinazotekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai – SLR, unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wametakiwa kuitisha mikutano ya mara kwa mara na Kamati za Maliasili na Mazingira za Vijiji, ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa mradi huo.
Rai hiyo imetolewa hii leo Desemba 8, 2023 na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda wakati akifungua mafunzo kwa Kamati za Maliasili na Mazingira kutoka Vijiji 20 vilivyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa zinazotekeleza mradi huo ikijumuisha Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga (Rukwa), Tanganyika (Katavi) na Mpimbwe (Katavi).
Amesema, ni wajibu wa Maafisa viungo kuhakikisha kamati za maliasili na mazingira za vijiji zinapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa Serikali za vijiji ili kuhakikisha kuwa elimu ya uhifadhi wa mazingira na urejeshaji wa uoto wa asili inawafikia wananchi wanufaika kupitia mradi huo.
“Nawahimiza Maafisa viungo kutambua umuhimu wa kufanya mikutano na kamati za maliasili na mazingira za vijiji pamoja na serikali za vijiji ili kuhakikisha kunakuwepo na uelewa wa kutosha kuhusu mradi huu ambao una manufaa makubwa kijamii na kiuchumi,” amesema Dkt. Mapunda.
Aidha Dkt. Mapunda pia amewataka maafisa viungo kuhakikisha viongozi wa kamati za maliasili na mazingira za vijiji wanatambua vyema jukumu lao katika usimamizi na utekelezaji wa mradi ili kuwawezesha wananchi kuendesha shughuli zao za kijamii na kiuchumi kupitia uvuvi, kilimo, ufugaji na kupata mazao yenye tija.
Amesema, mradi huo ulianzishwa mahsusi na serikali ikiwa ni juhudi za za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu zisizo rafiki na mazingira ikiwemo ukataji miti, uchomaji mkaa na uharibifu wa vyanzo vya maji ambavyo vimekuwa tishio kwa uhai wa binadamu na viumbe hai.
“Mradi pia umekusudia kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo tutawezesha uboreshaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo pamoja na malisho ya mifugo ili kuzuia muingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo vyanzo vya maji,” aliongeza Dkt. Mapunda.