Serikali Nchini Uganda imesema maafisa wa serikali watakaopatikana kuhusika na ufisadi, watachukuliwa hatua kali ikiwemo kufungwa jela.
Hayo yamesemwa na Rais wa Nchi hiyo Yoweri Museveni baada ya kukamatwa na kuzuiwa kwa mawaziri watatu, wanaodaiwa kuiba mabati yaliyopaswa kuwajengea makaazi watu masikini kutoka eneo la Karamoja.
Itakumbukwa mwezi machi Rais Musaveni aliagiza idara ya upelelezi DDP na polisi kuanzisha uchunguzi kuhusu madai ya utumizi mbaya wa mabati, yaliyolenga kuifaidi jamii katika eneo la Karamoja.
Mawaziri hao watatu walikamatwa akiwemo Mary Goreti Kitutu, Amos Lugolobi, wawili hawa wako nje kwa dhamana, wakati huu Agnes Nandutu akiendelea kuzuiliwa akisubiri kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo Aprili 27 Mahakama ilimzuia Joshua Abaho, kwa tuhuma sawia na hizo za utumizi mbaya wa mamlaka.
Wanasiasa wa upinzani wameendelea kuishtumu serikali ya rais Museveni kutochukua hatua kali dhidi ya watu wanaojihusisha na ufisadi.