Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limewateuwa Maafisa Watatu kutoka Mamlaka za Soka nchini Tanzania, kuelekea michezo ya Mzunguuko wanne wa Michuano ya Kimataifa upande wa Vilabu.
Mzunguuko wanne wa Michuano hiyo utapigwa juma lijalo, ambapo michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika imepangwa kupigwa Machi 07, 11 na 18, huku Michezo ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ikipangwa kupigwa Machi 08.
Taarifa kutoka ‘CAF’ imethibitisha kuteuliwa kwa Meneja Mashindano wa TFF, Baraka Kizuguto kuwa Mratibu (General Coordinator) wa mchezo wa Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya Mabingwa wa Afrika Kusini Mamelodi Sundowns dhidi ya vs Al Ahly SC ya Misri. utakaochezwa Machi 11.
Miamba hiyo ilikutana nchini Misri Jumamosi (Februari 25) na kuambulia matokeo ya 2-2.
Meneja wa Ligi (TPLB), Jonathan Kassano ameteuliwa na CAF kuwa Mratibu (General Coordinator) wa mchezo wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika Al Hilal (Sudani) vs Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) utakaochezwa Machi 18, 2023.
Mchezo uliopita uliozikutanisha timu hizo katika Uwanja wa Loftus Versfeld mjini Pretoria-Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns iliibuka na ushindi wa 1-0, bao likifungwa na Mailula dakika ya 25.
Afisa mwingine kutoka TFF aliyeteuliwa na CAF, ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Khalid Abdallah ambaye atakuwa Kamishna wa mchezo wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika Zamalek SC (Misri) vs E.S.T. (Tunisia) utakaochezwa Machi 7, 2023.
Mchezo uliopita wa Mzunguuko watatu ilishuhudiwa Zamalek SC (Misri) ikipigwa 2-0 ugenini katika Uwanja wa Hammadi Agrebi, mjini Tunis-Tunisia.