Wateule wa Rais watakiwa kuzingatia maeneo nane ya msingi, ikiwamo kujiamini katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Rais Samia katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa faragha uliowakutanisha mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali jijini Arusha.
“Lakini unapokuwa unajiamini hakikisha pia unakuwa tayari kuutetea uamuzi uliofanya, lingine ni kuendeleza rasilimali watu, hili ni eneo muhimu sana, usipopanga vizuri kwamba akitoka huyo miaka 60 huyu yupo anachukua nafasi kwa uhakika” amesema Rais Samia
“Usipowapanga vizuri, unapanga future ambayo haina future. Kila mmoja akijiamini anaweza kuchukua kazi ya bosi wake na kwenda nayo, basi unapanga future yenye future”.
“Tafuta watu wenye nia ya kufanya mambo yafanikiwe, usichukue watu ambao anakuja kuendeleza ile routine (ratiba) iliyozoeleka, leta watu wenye mawazo mapya, leta mtu atakayekusaidia kufikiri mambo mambo mapya ya taasisi yako”.
Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo wa mafunzo mahususi, Rais Samia ametaja eneo la tatu kuwa ni umuhimu wa kufanya kazi na sekta binafsi ili kupata mitaji mikubwa itakayosaidia katika utekelezaji wa miradi yenye kuongeza ajira, vyanzo vipya vya mapato na uzalishaji.
Nne, ni kuweka mbele ya masilahi ya Taifa katika jambo wanalohusika kwenye utekelezaji, kuongeza ubunifu katika utendaji wao, kuachana na utumwa wa sheria zinazokwamisha utekelezaji wa mipango iliyopo na kujenga utamaduni wa mawasiliano kwa njia ya mifumo ya serikalini.
Saba ni kuzingatia mafunzo huku akiagiza Taasisi ya Uongozi kurejesha utamaduni wa mafunzo kwa watendaji hao, utekelezaji wa mipango ya Serikali na utoaji wa taarifa hizo kwa wakati pamoja na kutathmini kiapo chao cha kulinda, kuhifadhi na kuitetea Katiba ya Jamuhuri ya Muungano.