Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo sita kwa viongozi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Umoja wa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri unaohusika na maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) yatakayosaidia kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati akifungua Mkutano wa 13 wa TOA (Tanzania Local Government Reforms Association) ulioanza Aprili 4, 2023 kwenye ukumbi wa Jiji, Mtumba, jijini Dodoma.
Amesema, viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wawashirikishe kwa karibu wa wananchi katika kuainisha changamoto zinazowakabili, na kuwawezesha kupanga na kutekeleza afua za kukabiliana na changamoto hizo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
“Kwa kufanya hivyo, tutaweza kutekeleza kwa tija, dhana ya ugatuzi wa madaraka sambamba na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana kwa wananchi yanakuwa dhahiri na endelevu,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Aidha, ameitaka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ihakikishe Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka inakamilika mara moja ili iwezeshe taasisi zote nchini kupata mwongozo wa namna ya kutekeleza dhana hii muhimu kwa utoaji wa huduma na maendeleo ya wananchi.
Ili kuwajengea uwezo wanachama wake, Waziri Mkuu pia ameitaka TOA iendelee kuweka mikakati ya kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na mifumo ya utatuzi wa migogoro sambamba na ushirikishaji wananchi katika maamuzi na mipango ya maendeleo.
Pia ameitaka TOA iweke kipaumbele kwa wanachama wake katika kuandaa mikakati ya usimamizi wa miradi ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kazi zinazofanywa ziwe na ubora na zilingane na fedha inayotumika.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema anatambua wapo watumishi wengi walionufaika na mpango wa mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa Osaka, Japan kuanzia mwaka 2002. Amesema anaamini waliopata bahati ya kuhudhuria mafunzo hayo, wameona na kujifunza kuwa Wajapan wanayo mifumo thabiti ya kuwashirikisha wananchi na kujenga uwezo kwa mamlaka zao za Serikali za Mitaa ili ziwahudumie ipasavyo.