Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation ya China inayojenga barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganga kuongeza kasi ya ya ujenzi ili waeze kukamilisha kwa wakati.
Ametoa agizo hilo leo Julai 26, 2021 alipokutana na viongozi hao na kufanya mazungumzo mbalimbali katika kijiji cha Namahema wilayani Ruangwa ikiwemo, barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 53.2 inatarajiwa kugharimu kiasi cha sh bilioni 59.28 ambapo umepangwa kukamilika Novemba 2022.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amesema barabara ya Ruangwa – Nanganga ni muhimu kwani kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo yakiwemo mazao mbalimbali ya kilimo hivyo kuchangia katika kukuza uchumi na kuongeza tija kwa wakulima.
Kwa upande wake, Meneja Mkaazi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation Bi Su Jinlan amemuhakikishia Waziri Mkuu wataongeza kasi ya ujenzi wa mradi wa barabara hiyo na kwamba itakamilika kwa wakati. Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 18 ya utekelezaji.
Sambamba na hayo yote Waziri Mkuu Majaliwa amezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Gogovivu wilayani Ruangwa nakuwahasa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.