Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, wawafuatilie na kuwarejesha Dodoma watumishi 11 waliokuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili wajibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kupora maeneo ya wananchi na kugawa maeneo ya wazi.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo, kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo.

Amesema, “Watumishi wa Jiji la Dodoma ni Josephat Mafuru (aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji), Scorpion Philip, Lennis Ngole, Allen Mwakanjuki, Aisha Masanja, Agusta Primo, Azory William Byakanwa, Frezia Kazimoto, Premin Nzenga, Stella Komba na Thabiti Mbiyagi. Hawa ni wachache miongoni mwa wengi waliohusika kusababisha migogoro, watafutwe na waje kujibu tuhuma dhidi yao.”

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa.

Majaliwa amesema, Jiji la Dodoma litekeleze mapendekezo ya Kamati Maalum ya Uchunguzi kwa kufanya uhakiki wa hati pandikizi zote, litafute maeneo na kuwafidia wananchi wanaolidai Jiji na liwe limekamilisha utekelezaji ifikapo Januari 30, 2024.

Aidha, ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi wajiridhishe kuhusu matumizi ya fedha za Mkopo wa Mradi wa KKK sh. bilioni moja zilizotumika kulipa fidia ili kupisha upanuzi wa ujenzi wa hoteli ya Jiji (Dodoma City Hotel) iliyoko mtaa wa Uhindini.  

Ameagiza maeneo yote ya umma ikiwemo shule, vituo vya afya, bustani za kupumzikia na masoko, yasibadilishwe matumizi yake hadi yaidhinishwe na Kamati za Usalama za Wilaya na Mikoa kama ipo haja ya kufanya hivyo na kuridhiwa na Waziri wa Ardhi, baada ya kupokea muhtasari wa Kamati ya Usalama ya Mkoa.

Kilele mbio za Mwenge: Twange awapa neno Wananchi
Zlatan Ibrahimovic: Hana uzoefu na timu kubwa