Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), MaaliM Seif Sharif Hamad amezungumzia sababu zilizomfanya yeye na timu yake kujiunga na ACT-Wazalendo ingawa alipewa nafasi na vyama vingine vya upinzani.
Mwanasiasa huyo mkongwe ameeleza sababu za kufanya machaguo hayo wakati ambapo wengi waliamini huenda angejiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hasa kutokana na kuwa na ushirikiano wa karibu na chama hicho tangu mwanzo wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Akijibu swali la mwandishi wa habari katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya jana kutangaza uamuzi huo, Maalim Seif alisema kuwa waligonga hodi katika vyama kadhaa vya upinzani na walikaribishwa vizuri, lakini baada ya kuzipitia katiba zao na kufanya uchambuzi wa masharti waliyopewa waliona ACT-Wazalendo itawafaa zaidi.
“Kabla ya kuchukua maamuzi haya tulitembelea baadhi ya vyama ili kuwaambia ‘ikitokea sisi kuhama.. Je, mko tayari kutukaribisha? Na mko tayari kutukaribisha kwa masharti gani?’ Vyama tulivyovitembelea vilituonesha kwamba viko tayari kutukaribisha,” alisema Maalim Seif.
“Lakini ukija sasa kwenye yale masharti, ambayo unatukaribisha kwa masharti gani… tukakaa na tukaamua kwamba kwa yale yote basi ACT-Wazalendo hawa kwakweli masharti yao sio magumu, tukasoma Katiba zao na tukaona Katiba ya ACT-Wazalendo inatufaa sisi kwahiyo tukaamua kwenda huko,” aliongeza.
Baada ya kuchukua uamuzi huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Vincent Mashinji alimpongeza na kumtakia kila la kheri katika chama chake hicho kipya, huku akiamini watashirikiana.
Katika hatua nyingine, Maalim Seif ambaye anaamini katika itikadi tofauti na Ujamaa unaohubiriwa na chama chake kipya, alisema kuwa walizungumza na uongozi wa chama hicho ambao walieleza kuwa suala hilo linazungumzika na kwamba watafikia muafaka.
Aidha, alieleza kuwa yeye na wenzake wameamua kuhamia ACT-Wazalendo bila kuweka masharti yoyote ya kupewa nafasi za uongozi na kwamba yeye yuko tayari kuwa mwanachama wa kawaida ili mradi tu aendelee na mapambano ya kisiasa.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameeleza kuwa kilichomtokea Maalim Seif ni sehemu ya mapambano.
“Maalim na timu yake ni sehemu muhimu sana katika haya mapambano, tunamtakia kila la kheri,” Mwananchi wanamkariri Mbowe.
Maalim Seif na wenzake walitangaza kuachana na CUF saa chache baada ya Mahakama Kuu kuhalalisha uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho. Hivi karibuni, Profesa Lipumba alimvua Ukatibu Mkuu Maalim Seif baada ya kuchaguliwa tena kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano.