Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mstaafu, Maalim Seif Sharif Hamad jana aligoma kumpa mkono Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Tukio hilo lilitokea katika mazishi ya Rais wa zamani wa Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi yaliofanyika jana katika eneo la Migombani visiwani humo.

Dk. Shein ambaye alikuwa akiwaongoza viongozi wa kitaifa katika msiba huo alianza kwa kusalimiana na viongozi wengine kama ishara ya kupeana pole lakini alipofika kwa Maalim Seif hali ilikuwa tofauti. Rais huyo wa Zanzibar alionekana kushtushwa na kukataliwa kwa mara ya kwanza na kuamua kurudia kwa mara ya pili lakini Maalim Seif aliendelea kugoma.

Viongozi wa dini na Serikali wakimsindiza Mzee Jumbe kwenye safari yake ya mwisho

Viongozi wa dini na Serikali wakimsindiza Mzee Aboud Jumbe kwenye safari yake ya mwisho

Viongozi mbalimbali waliokuwa karibu walisikika wakiguna kwa mshangao kwani hawakutegemea uhasimu wa kisiasa kufikia hatua hiyo.

Hata hivyo, Dk. Shein alikubaliana na kile alichokiona na kuamua kuendelea kuwasalimu viongozi wengine waliofuata.

Kitendo hicho cha Maalim Seif kinatafsiriwa kama sehemu ya utekelezaji wa maamuzi ya CUF kutoshirikiana na viongozi wa Serikali ya Zanzibar ambao imekuwa ikidai uliingia madarakani kwa kukwapua ushindi wa upande huo wa upinzani.

CUF imekuwa ikihamasisha wananchi wake kutoshirikiana na Serikali ya Zanzibar wakipinga hatua ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana na kuitisha Uchaguzi wa Marudio ambao chama hicho kiliususia na kupelekea CCM kushinda kwa zaidi ya asilimia 90.

Wakati Maalim Seif akikataa kumshika mkono Dk. Shein, aliendelea kusalimiana na viongozi wengine wa CCM na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waliohudhuria msiba huo.

Mzee Aboud Jumbe alizikwa kwa utaratibu kama mwananchi wa kawaida, hakukuwa na milio ya mizinga wala mwili wake haukubebwa kwenye magari ya Jeshi, ikielezwa na familia kuwa hayo yalikuwa maelekezo ya wosia wake.

Kubenea ajisalimisha Polisi kwa uchochezi
Video: Wizara Ya Maliasili Na Utalii Kuchangia Ukuaji Wa Pato La Taifa