Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa anajipanga kuwasilisha majina ya wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini ya chama hicho na kuiwasilisha kwa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA).
Uamuzi huo wa Maalim Seif umekuja ikiwa ni siku moja baada ya Mahakama Kuu kubatilisha uteuzi wa wajumbe wa bodi ya udhamini waliokuwa wamechaguliwa na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na wajumbe wapya aliokuwa amewawasilisha Katibu Mkuu huyo.
Uamuzi wa Mahakama ulisababisha kuendelea kutambulika kwa wajumbe waliokuwepo awali, licha ya muda wao kuwa umekwisha. Hivi sasa chama hicho kinapaswa kuwa na wajumbe wapya.
“Tutafanya uteuzi mpya wa wajumbe wa Bodi kwa kufuata vifungu vyote vya sheria na tutawapeleka RITA ili Bodi isajiliwe. Ni matumaini yangu RITA itafanya kazi kwa mujibu wa sheria,” Maalim Seif amewaambia waandishi wa habari.
Ameeleza kuwa uamuzi wa Mahakama umewapa nguvu na ari wanachama wa CUF ambao walikuwa wamevunjika moyo kutokana na mgogoro uliokuwa unakipasua chama hicho.
Mgogoro ndani ya CUF ulianza miezi kadhaa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2015, ambao ulifanyika huku Profesa Lipumba akiwa amewasilisha barua ya kujiuzulu.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alirejea baadaye na kuahirisha uamuzi wake, hali iliyozua mgogoro wa utambulisho wake kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa chama hicho.
Hivi sasa, umoja wa chama hicho umekuwa ukitafunwa na makundi ya Timu Lipumba na Timu Maalim Seif.