‘Timuatimua’ ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) inaendelea kufuatia mgogoro wa chama hicho uliozaa kambi mbili pinzani. Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza kuwafukuza rasmi uachama Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma ambao wote ni ‘Timu Lipumba’.
Hatua hiyo imebainika kufuatia barua ya tarehe 29 mwezi Julai mwaka huu iliyoandikwa na Maalim Seif kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na kutuma nakala kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Katika barua hiyo, Maalim Seif alieleza kuwa Baraza Kuu la chama hicho lilifanya kikao cha dharura Julai 28 mwaka huu na kufikia uamuzi wa kuwavua uanachama wabunge hao wawili kutokana na vitendo vya kukihujumu chama hicho.
- Video: Rais Magufuli akiwasili Tanga, kuelekea uzinduzi wa bomba la mafuta
- Magazeti ya Tanzania leo Agosti 3, 2017
Alisema kuwa katika kikao hicho, wajumbe 43 kati ya wajumbe 45 walipiga kura ya kuridhia kufukuzwa kwa wabunge hao ikiwa ni sawa na asilimia 95.5 ya kura zote zilizopigwa kwa siri. Hivyo, alimtaarifu Spika kuwa kutokana na uamuzi huo wa Baraza Kuu, Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara na Nachuma wanapoteza sifa za kuendelea kuwa wabunge.
“Kwa kufukuzwa uanachama, Sayaka na Nachuma wamepoteza sifa za kuwa wabunge na naomba uchukue hatua za kuwavua ubunge,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Hata hivyo, Ofisi ya Bunge kupitia kwa Kaimu Katibu wake, Nenelwa Mwihambi imeeleza kuwa bado haijaipata barua hiyo.
Uamuzi huo wa Maalim Seif umekuja ikiwa ni siku chache baada ya Profesa Lipumba kutangaza kuwafukuza uachama wabunge nane wa viti maalum wa chama hicho, uamuzi ambao uliridhiwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na NEC wakapitisha majina mapya ya wateule yaliyowasilishwa kujaza nafasi hizo.
Wabunge nane waliotimuliwa na Kambi ya Profesa Lipumba wamefungua shauri mahamani kupinga kuapishwa kwa wabunge wateule hadi mahakama itakapomaliza kusikiliza shauri lao la msingi la kupingwa kuvuliwa uanachama na kung’olewa katika nafasi zao za ubunge wa viti maalum.