Hatimaye, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametoa msimamo wake na chama chake kufuatia mazungumzo ya siri ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hotel ya kitalii ya Serena jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesisitiza kuwa hoja ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar kama inavyoelezwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina msingi, haikubaliki na sio halali kikatiba.

“Hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo na vurugu na inaweza kuleta mzozo mkubwa wa kikatiba wa kisheria. Sidhani kama tunataka kuwapeleka huko watanzania,” alisema Maalim Seif.

Makamo huyo wa kwanza wa rais wa Zanzibar alieleza kuwa tayari wameshafanya vikao nane vilivyowashirikisha wagombea urais pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar lakini hawakukubaliana na kurudiwa kwa uchaguzi kama baadhi ya viongozi wa CCM walivyoeleza.

Aidha, Maalim Seif alikanusha kilichoelezwa na Makamo wa Pili wa rais Balozi Seif Ali Idd baada ya kukutana na rais John Magufuli, kuwa rais alisema warudi Zanzibar kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwani rais hakusema hivyo alipokutana naye.

Maalim Seif alisema kuwa ana imani kubwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika kuleta maridhiano na ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar kutokana na mazungumzo aliyofanya naye hivi karibuni katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa endapo uchaguzi mkuu utatakiwa kurudiwa, zipo changamoto nyingi za kikatiba ambazo zitakwamisha zoezi hilo hivyo uchaguzi huo hautawezekana. Alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa fedha za kugharamia uchaguzi na baraza la wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa limefikia ukomo wake.

Alisema kuwa njia nyingine ingekuwa kwa wajumbe wa baraza kujiuzulu, lakini hawawezi kufanya hivyo kwakuwa wao hawakufanya kosa bali kosa lilifanywa na Jecha Salum Jecha binafsi.

Mbali na hilo, Maalim Seif alieleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa kutoa tamko lisilo halali la kufuta uchaguzi huo huku akifahamu dhahiri kuwa hana nguvu hiyo kikatiba.

Aliitaka ZEC iongozwe na makamu mwenyekiti wake kwa mujibu wa katiba pamoja na wajumbe wengine kukamilisha utaratibu wa kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi.

Hata hivyo, Maalim Seif alieleza kuwa anafahamu dhahiri kuwa kuna mpango wa kutangaza kwa nguvu marudio ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, lakini yeye pamoja na chama chake hawatakubali.

Tanzia: Leticia Nyerere afariki
Tuchel: Aubameyang Hauzwi Kwa Gharama Yoyote