Mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anadai kuwa mshindi wa nafasi hiyo kufuatia matokeo aliyoyajumuisha kutoka vituoni, ameeleza kuwa ikifikia kesho (November 2) kama ZEC watakuwa hawajamtangaza kuwa mshindi ataachana na jambo hilo.

Kupitia taarifa yake aliyoituma Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maalim Seif ameeleza kuwa kwa kuwa Katiba ya Zanzibar inaonesha kuwa kesho ndio ukomo wa Rais Ali Shein kuongoza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba kuendelea itakuwa ni mgogoro wa kikatiba, yeye ataliachia suala hilo mikononi mwa wanananchi.

Alisema kuwa hana nia yoyote ya kuiingiza Zanzibar katika machafuko ya aina yoyote na kwamba anahimiza amani idumu lakini pia haki itendeke bila kumpendelea mtu yeyote.

Alieleza kuwa ameshafanya juhudi za kutaka kutatua mzozo huo kwa kumtafuta Dkt. Ali Shein pamoja na Rais Jakaya Kikwete lakini juhudi zake zilishindikana baada ya kutopewa ushirikiano na wasaidizi wa marais hao. Alisema hali ilikuwa hivyo pia alipotaka kufanya mashauriano na ZEC.

Pamoja na mambo mengine, Maalim alieleza kushangazwa na uamuzi wa NEC kuyakubali matokeo ya majimbo 18 ya Pemba ambayo ZEC ilidai yana kasoro kubwa. Pia, alidai kupokea taarifa kuwa mwenyekiti wa ZEC pamoja na baadhi ya wajumbe walikaa kikao viongozi wa CCM na kuwataka kupinga matokeo.

CUF waliwaahidi wananchi kuwa watafanya kazi ya kuliongoza taifa hilo kwa amani na kushirikiana na viongozi wa CCM kupitia serikali ya umoja wa kitaifa kwa mujibu wa katiba na kwamba haitawabagua watu kwa misingi ya udini, ukabila au itikadi zao za vyama.

Ikulu Yakanusha Madai Ya Maalim Seif
Lowassa Asema Anajipanga Upya, Ukawa Kuhamishia Kambi Zanzibar