Viongozi kutoka vyama vya upinzani nchini vya Chadema na CUF, Edward Lowassa na Maalim Seif Sharif Hamad wamemnadi mgombea ubunge Jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhan na kulalamikia utawala uliopo madarakani kuwa unaendesha mambo kibabe.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za mgombea huyo kwenye Skuli ya Fuoni, Zanzibar, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu CUF, amesema chanzo cha mgogoro wa Zanzibar kuhusu Uchaguzi Mkuu uliopita ni Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Aidha, Maalim amesema wanachama wa CUF walivunjika moyo kutokana na kauli ya Kinana akidai kuwa kiongozi huyo wa CCM hajui chochote kinachoendelea nchini.
“Wengi wametishika na kauli ya Kinana hajui chochote kinachoendelea katika nchi na hata chama chake,mwacheni mwenyewe,”amesema Maalim.
Kwa upande wake Edward Lowassa, amewashukuru Wazanzibar kwa mahaba yao ya kumpa kura wakati wa uchaguzi mkuu wa urais uliopita.
“Nawashukuru sana kwa mahaba yenu kwani yameonekana Wazanzibar asanteni sana, baada ya uchaguzi tulizuiwa kufanya mikutano,lakini Maalim Seif alifanya kazi kubwa sana, walikuwa wakimfuata kila sehemu hata misikitini, lakini hawamuwezi,”amesema Lowassa.
Hata hivyo, Lowassa amesema alishindwa kwenda visiwani Zanzibar kwakuwa mikutano ya hadhara ilizuiwa kwa vyama vya siasa.