Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF) anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Maalim Seif Sharif ameahidi kuirudisha bungeni rasimu ya katiba mpya iliyowasilishwa na tume ya iliyoongozwa na Jaji Warioba ikibeba maoni ya wananchi.

Maalim Seif alitoa ahadi hiyo jana katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake katika visiwa vya Zanzibar, mkutano ambao ulihudhuriwa na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.

Aliwataka wananchi kuwapigia kura yeye na Lowassa kwa nafasi ya urais kwa kuwa tayari wamekubaliana kushirikiana kuirudisha bungeni rasimu ya katiba ya Jaji Warioba iliyopendekeza Muundo wa Muungano wa serikali tatu.

“Mlio wengi mlitaka muungano wa mkataba lakini tume wakasema tupate serikali tatu, kwa bahati mbaya CCM waliikataa na kuweka vitu vyao,” alisema.

“Hata waliokuwa mbele katika mambo hayo walishindwa kuitetea Zanzibar na badala yake walipofika huko waliufyata wakaandaa rasimu yao wakakubali Zanzibar iendelee kudhalilishwa,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Mgombea huyo aliahidi kuwa serikali yake itahakikisha wananchi wote wa Zanzibar wanapata ajira ndani ya kipindi cha miaka mitano. Alisema atahakikisha uchumi wa nchi hiyo unakuwa imara zaidi kama wa nchi ya Singapole.

Aidha, Maalim Seif aliahidi kuwarudisha katika magereza ya Zanzibar Mashehe wa Uamsho wanaoshikiliwa katika magereza ya jiji la Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka ya uchochezi.

Kwa upande wake Edward Lowassa, aliwataka wananchi kuwachagua ili walete mabadiliko makubwa ya kimaendeleo nchini huku akiwasihi wananchi kuwa wavumilivu kwa kutochana mabango ya wagombea wa vyama vingine kwa kuwa huu ni wakati wa kampeni.

Aliwataka wananchi kuwapigia kura na kuhakikisha wanachunga kura zao, “wangapi watamchagua Lowassa, wanyooshe mikono juu…uwezo wa kushinda tunao, ninawaambia CCM waache kuiba kura,” alisema.

Twiga Stars Yashindwa Congo Brazzaville
Ester Bulaya Amuokoa Mtoto Wa Wasira Kuchomwa Moto