Serikali nchini China leo Februari 16, 2020 imeripoti juu ya kupungua maambukizi mapya ya virusi vya corona kwa siku ya tatu mfululizo wakati ikibainika kuwa uongozi wa taifa hilo ulifahamu ukubwa wa kitisho cha virusi hivyo hata kabla ya kutolewa kwa tahadhari.
Tume ya afya ya China imesema kumekuwa na visa vipya 2,009 pekee upande wa China bara na kufanya idadi ya walioambukizwa virusi hivyo kufikia 68,500.
Kiwango cha vifo hakijapungua baada ya kurekodiwa vifo vipya 142 na kufikisha idadi ya waliokufa kutokana na ugonjwa COVID-19 kuwa watu 1,665.
Mripuko wa virusi vya Coorna ulianzia kwenye mji wa Wuhan ulio katikati ya jimbo la kati ya China la Hubei na tangu wakati huo virusi hivyo vimesambaa kwenye mataifa zaidi ya 24 na kuzusha wasiwasi mkubwa wa kiafya.