Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema maambukizi ya homa ya ini yamepanda kutoka asilimia 4.0 mpaka kufikia asilimia 7.8. Ameyasema hayo jana katika maadhimisho ya siku ya homa ya ini duniani Julai 29.
Amesema kuwa “Takwimu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) zinaonyesha hali ya maambukizi ya homa ya ini aina ya B na C kwa mwaka 2018/2019 ni asilimia 5.9 kwa B na C imefikia asilimia 1.9″na hivyo kufikisha maambukizi ya asilimia 7.8.
Aidha Mwalimu amebainisha kuwa Wizara imekuwa ikiratibu utoaji wa chanjo ya homa ya ini B bila malipo kwa watoto kuanzia mwaka 2002 hadi kuifikia mwaka 2019 na zaidi ya watanzania millioni 20 walio chini ya umri wa miaka 17 wamepatiwa chanjo.
Chanjo hiyo hutolewa katika hospitali za rufaa ngazi ya taifa, hospitali 27 za mikoa na baadhi ya hospitali za halmashauri na vituo 21 vilivyopo mipakani.
Aidha huduma ya chanjo kwa watu wazima inatolewa kwa bei elekezi ya serikali ambapo gharama ya kipimo ni shillingi 10000 na chanjo kwa kila dozi ni shilingi 10000 na dozi hitaji ni tatu.