Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Saa 72) iliyokutana jana Januari 25, 2018 imejadili mechi mbalimbali za Ligi Kuu (VPL) Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL).
Mechi namba 95 (Mbeya City 1 vs Kagera Sugar 1). Klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 1, 2018 jijini Mbeya, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu.
Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Bodi ya Ligi kutoa waraka kwa wamiliki wa viwanja kuhakikisha timu zinaingia uwanjani kwa kutumia milango rasmi tu.
Mechi namba 100 (Tanzania Prisons 3 vs Mbeya City 2). Kocha wa Mbeya City, Ramadhani Mwazurimo amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano), adhabu ambayo imezingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Kocha Mwazurimo aliondolewa kwenye benchi (ordered off) na Mwamuzi baada ya kumtolea lugha ya kashfa katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 14, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Pia klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwa madai alikataa kutoa penalti kwa timu hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Kamati imeteua wajumbe watatu kupitia mkanda wa mechi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine itachunguza kiwango cha uchezeshaji cha Mwamuzi wa mechi hiyo, Bw. Israel Nkongo na kuwasilisha taarifa yake kwa ajili ya hatua zaidi.
Mechi namba 103 (Majimaji 1 vs Azam 1). Klabu ya Azam FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kukataa wachezaji wake wakaguliwe ndani kwa madai kuwa chumba kimepuliziwa dawa katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 18, 2018 Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kitendo cha timu hiyo ni kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yao imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia klabu hiyo imeandikiwa barua ya kutakiwa kuthibitisha madai yake kuwa chumba hicho kilikuwa kimepuliziwa dawa.
Mechi namba 104 (Simba 4 vs Singida United 0).Mtunza Vifaa wa Singida United FC, Mussa Rajab amefungiwa mwezi mmoja na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kutokana na kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mapumziko na kumlalamikia mwamuzi.
Kitendo alichofanya Mtunza Vifaa huyo katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 18, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kimekiuka Kanuni ya 14(10) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 41(2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Viongozi.
Mechi namba 106 (Mbao 0 vs Stand United 1). Klabu ya Stand United imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) kwa dakika sita, na pia kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika tisa katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 20, 2018 Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Adhabu kwa klabu hiyo iliyokiuka Kanuni ya 14(2a) ya Ligi Kuu, imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 112 (Kagera Sugar 0 vs Simba 2). Suala la mchezaji wa Kagera Sugar, Juma Nyoso kumpiga shabiki baada ya mechi hiyo iliyochezwa Januari 22, 2018 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kumalizika, limepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.