Serikali imesema, shughuli za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2024 zitaendelea.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim majaliwa Bungeni jijini Dodoma mapema wiki hii na kuongeza kuwa, kazi zitakazofanyika ni pamoja na kulifanyia maboresho Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; kuboresha mifumo ya menejimenti ya uchaguzi.
Amesema, kazi nyingine ni pamoja na kuendelea na mchakato wa marekebisho ya sheria za uchaguzi; kuandaa kanuni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi.
Majaliwa amesema, “Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa vyama vya siasa kuhamasisha Wanachama na Watanzania wote wenye sifa kujiandikisha kwenye daftari hilo na kupata kitambulisho halali cha mpiga kura pale zoezi hilo litakapoanza rasmi.”