Idadi ya vifo vya watu inazidi kuongezeka nchini Iraq kufuatia maandamano yaliyozuka siku nne zilizopita ya kupinga Serikali ya nchi hiyo. Imeripotiwa kuwa watu 60 wamepoteza maisha na mamia wamejeruhiwa.
Idadi hiyo ni ongezeko maradufu ndani ya saa 24 zilizopita baada ya waandamanaji kupambana na askari polisi waliokuwa wanatuliza ghasia.
Jeshi la nchi hiyo limeeleza kuwa kumekuwa na kundi la wadunguaji wasiojulikana wanaoua raia na maafisa wa polisi jijini Baghdad.
Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdel Mahdi ameeleza kuwa Serikali yake imeyasikia mahitaji ya waandamanaji hao na inayafanyia kazi. Hivyo, amewasihi kuwa watulivu.
Tangu Jumanne wiki hii, waandamanaji hao walianza kupinga hali ya kukosekana kwa ajira hasa kwa vijana kwa kiwango cha juu, huduma kwa umma zisizoridhisha pamoja na ufisadi wa hali ya juu.
Maandamano hayo yamekuwa changamoto ya kwanza kubwa kwa Serikali ya Mahdi, ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu aingie madarakani. Kiongozi huyo amewasihi wananchi kutounga mkono maandamano hayo akieleza kuwa hakutakuwa na muujiza wa kupata suluhu.
Hata hivyo, licha ya kuwepo juhudu kubwa za kutuliza maandamano hayo, mamia ya wananchi wameongezeka mtaani kuunga mkono maandamano hayo jana ikiwa ni saa chache tangu Serikali izime mtandao.
Kwa mujibu wa Reuters, Polisi wamekuwa wakifyatua risasi kuwazuia waandamanaji wasiendelee na safari yao ya kujaribu kufika katikati ya jiji la Baghdad, eneo la Tahrir Square ambalo wamepania kuweka kambi.