Maandamano makubwa yameibuka nchini Sudan kupinga kuongezeka kwa ugumu wa maisha na kupanda kwa gharama za bidhaa. Serikali ya nchi hiyo imetangaza hali ya dharura kufuatia maandamano hayo yanayohusisha mamia ya wananchi.
Madaktari nchini humo wanadaiwa kupanga kuungana na waandamanaji, baada ya kutibu idadi kubwa ya majeruhi wa maandamano yanayopinga Serikali ya Rais Omar al-Bashir.
Jana, kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo alidai kuwa waandamanaji 22 waliuawa na vyombo vya usalama. Hata hivyo, Serikali imepinga idadi hiyo iliyotajwa ingawa haikutaja idadi husika.
Maandamano nchini humo yalianza Jumatano wiki hii baada ya kutangazwa kwa ongezeko la bei ya mikate na mafuta.
Kwa miaka kadhaa, bei za vitu zimekuwa zikiongezeka mara dufu, mfumuko wa bei umepanda karibu asilimia 70 huku thamani ya fedha ya Sudan ikiwa inaporomoka.
Jumamosi, vyombo vya usalama viliwakamata viongozi 14 wa chama cha National Consensus Forces ambacho ni chama cha upinzani. Kiongozi wa chama hicho, Farouk Abu Issa ambaye ana umri wa miaka 85 pia ameripotiwa kukamatwa.
“Tunataka waachiwe mara moja. Tunajua kukamatwa kwao ni jitihada za kutaka kuyazima maandamano yaliyoko mitaani,” alisema Sadiq Youssef, msemaji wa chama cha upinzani.
Upinzani umedai kuwa maandamano hayo hayachochewi na wao bali ni hali ya maisha kuwa ngumu.
Rais al-Bashir anakumbwa na vikwazo kutoka katika nchi za Magharibi ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza.
Mataifa hayo yamemuweka katika orodha ya viongozi wanaotakiwa kukamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).