Jeshi la polisi nchini Nigeria limewatia mbaroni na kuwazuilia makumi ya watoto wa wanachama wa Harakati ya Kiislamu za nchi hiyo kwa zaidi ya siku mbili sasa.
Vyombo vya usalama nchini humo havijatoa maelezo ya kina na sababu za kukamatwa watoto hao ambao kimsingi wanapaswa kulindwa na sheria.
Watetezi wa haki za binadamu nchini humo wamelaani vikali kitendo hicho cha kukamatwa na kuzuiliwa watoto wadogo nchini humo.
Mara kwa mara watoto hao wamekuwa wakiandamana na wananchi Waislamu wa Nigeria katika maandamano ya kutaka kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye amewekwa kizuizini tokea mwaka 2015 aachiliwe huru.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa na kuwekwa kizuizini tarehe 13 Desemba 2015, wakati askari walipovamia na kufanya kumshikilia kwa tuhuma dhidi ya sakata la Hussainiyyah la mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo.
Mnamo mwezi Desemba 2016, Mahakama Kuu nchini humo ilitoa hukumu ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru mara moja, sambamba na kulitaka jeshi la polisi na vyombo vya usalama viilipe familia yake fidia ya dola laki moja na nusu, lakini polisi wameendelea kumshikilia kizuizini kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe licha ya kuripotiwa kudhoofika kwa Hali yake kiafya.