Siku moja baada ya baraza kuu la shirikisho la soka duniani FIFA kupitisha maamuzi ya kuongeza timu shiriki katika fainali za kombe la dunia kutoka timu 32 hadi 48, mwandishi wa michezo kutoka nchini Ireland Desmond Kane amekosoa uamuzi huo.
Kane ambaye ni mwandishi wa habari maarufu duniani, amesema maamuzi ya baraza kuu la FIFA kupitisha azimio la ongezeko la timu shiriki, yanaondoa uhalisia wa ushindani katika fainali za kombe la dunia.
Amesema ushindani katika fainali hizo ulipaswa kuendelea kama ilivyo sasa, ambapo timu za mataifa yote duniani huanza kushiriki katika hatua ya kuwania kufuzu, kwa kigezo cha nafasi 32 za ushiriki.
Amesema ufanisi mkubwa wa makocha na wachezaji ulikua unaonyesha uhalisia wa fainali za kombe la dunia kwa kila mmoja kutaka kushiriki, lakini kwa maamuzi ya kuongezwa kwa timu shiriki huenda baadhi ya timu zikabweteka kwa kuamini ni rahisi kupenya na kutinga katika fainali hizo.
Mfumo mpya wa ongezeko la timu shiriki unatarajia kuanza kufanya kazi kunzia fainali za kombe la dunia za mwaka 2026, ambazo bado hazijapata mwenyeji.
Tayari nchi za Marekani, Canada na Mexico zimeshatuma maombi ya kuwania nafasi ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo.
Mfumo huo utawezesha fainali za kombe la dunia kuwa na makundi 16 na kila kundi litakua na timu tatu. Timu mbili katika kila kundi zitafuzu kucheza hatua ya mtoano ya 32 bora.
Juma ya michezo 80 itachezwa katika fainali za kombe la dunia kwa kipindi cha siku 32.