Nchi za Afrika, Caribbean na Pasific (OACPS) zimehimizana kuimarisha ushirikiano wa kibiashara miongoni mwao, baada ya kutokea mabadiliko ya kiitikadi na janga la Corona katika Nchi za Ulaya,  jambo linalozifanya nchi wahisani kupunguza misaada au kutoa misaada yenye masharti magumu.

Akifungua Mkutano wa 111 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific unaofanyika kwa njia ya mtandao, Rais wa Baraza la hilo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema kutokana na mabadiliko ya nyakati Jumuiya hiyo inapaswa kuongeza ushirikiano wa kibiashara,rasilimali watu,ulinzi na usalama miongoni mwao kuliko wakati wowote hasa baada ya kutokea mabadiliko katika nchi za Jumuiya ya Ulaya…

Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 45 tangu Jumuiya hiyo yenye  wanachama 79 ianzishwe imeshakomaa vya kutosha na hivyo ni muda muafaka sasa kuangalia na kujenga mfumo mpya wa uchumi,siasa,biashara,ulinzi na usalama,misaada na mahusiano ambao utakuwa na haki zaidi na manufaa kati ya Jumuiya hiyo na Nchi za Jumuiya ya Ulaya.

Aidha Prof. Kabudi ameongeza kuwa idadi ya nchi inazounda Jumuiya hiyo ya Afrika,Caribbean na Pacific ni idadi tosha katika Umoja wa Mataifa na kwamba nchi hizo zikisimama kwa pamoja katika Umoja wa Mataifa zitasukuma ajenda nyingi zenye maslahi kwa Mabara na Nchi za Umoja huo.

Baadhii ya ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo wa siku tatu ni pamoja na nchi za OACPS kujadili namna ya kukuza na kuboresha Ushirikiano, kuongeza Wadau wake kama vile nchi za BRICS na kufanya mapitio ya mkataba mpya wa ushirikiano kati ya Nchi za Africa, Caribbean, Pasific na Ulaya kwa kuwa Mkataba wa sasa (Cotonou Partnership Agreement) unafikia kikomo.

“Wakati umefika sasa kwa Jumuiya hii kuongeza wadau, kushikamana na kusimama pamoja katika masuala muhimu ya kidunia kwenye jukwaa la Umoja wa Kimataifa, ajenda nyingine itakayo jadiliwa ni kuhusu muundo mpya wa Sekretarieti ya Jumuiya, unaolenga kuongeza uafanisi zaidi na kupunguza gharama za uendeshaji” amesema Prof. Kabudi.

Mkutano huo pia unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya biashara baina Afrika, Caribbean, Pasific na nchi za Jumuiya ya Ulaya likiwemo suala viwango vipya vya ushuru wa mazao ya samaki ambayo nchi Wanachama wa OACPS zimekuwa zikiuza kwenye soko  la Ulaya.

Dkt. Mwinyi avunja bodi ya Wakurugenzi
KMC FC kuivaa Simba SC kwa Mkapa

Comments

comments