Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Manyinyi Mathayo amewataka Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi Mkoani humo, kuitumia vyema elimu waliyoipata katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa utendaji kazi kuleta mabadiliko ndani ya Jeshi na jamii kwa ujumla.
Mbunge Manyinyi ameyasema hayo katika viwanja vya Kikosi cha Kutuliza Ghasia Kamnyonge, wakati akifunga mafunzo ya utayari awamu ya pili kwa wakaguzi na wakaguzi wasaidizi wa Polisi 32, kutoka Wilaya za Serengeti, Bunda, Butiama na Musoma na kuwataka wawe na utayari kimwili na kiakili ili kukabiliana na changamoto mbalimbali kabla, wakati na baada ya chaguzi zijazo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salim Morcase alisema mafunzo hayo ni endelevu yenye kuwajengea uwezo wa utendaji wao wa kazi katika kuwaongoza askari, kufanya kazi kwa weledi na kusimamia nidhamu kwa askari wanaowaongoza.
Akizungumza kwa niaba ya Wanafunzi, Mkaguzi wa Polisi, Frank Kaijage aliushukuru Uongozi wa Polisi Mkoa wa Mara kwa kuendesha mafunzo hayo na kusema walivyoingia ni tofauti na wanavyotoka, hivyo watatumia vizuri elimu waliyoipata kwa malengo kusudiwa.