Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema, serikali inajiandaa kuwasilisha Bungeni mabadiliko ya vipengele vya Sheria ya Habari, ili wabunge wakiridhia, utekelezaji wake uweze kufanyika.
Msigwa ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), uliofanyika katika Ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa anatambua tasnia ya habari ina changamoto kadhaa ikiwemo sheria zinazohitaji kurekebishwa.
Amesema, “Kwa sasa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria hii ili wabunge wakiridhia, tuendelee na utekelezaji wake. mchakato wa kukutana na wadau kwa ajili ya majadiliano ya vipengele vya sheria hiyo ya mweaka 2016, umekamilika.”
Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), alisema, “Niwahakikishie kuwa, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa vyombo vya habari kufanya kazi bila bughudha yoyote.”
Aidha ameongeza kuwa, “Tayari Mheshimiwa Rais ameshamuagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kukutana na wadau wa sekta ya habari na kujadili namna ya kuziboresha sheria ambazo siyo rafiki kwa tasnia ya habari,miongoni mwa sheria hizo ni ile ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016, ambapo tayari vikao kadhaa kati ya serikali na wadau vimefanyika.”
Hata hivyo Msigwa amefafanua kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wa habari ili kukabili changamoto zilizopo na kusema, “tutashughulikia changamoto zote zinazowakabili waandishi wa habari na kutatua sheria zisizo rafiki, ili kuwa na sheria zinazotokana na pande mbili kukubaliana yaani serikali na wadau.”