Mabaki ya machapisho ya Biblia ya kale yamepatikana katika kile ambacho maafisa wametaja kuwa “uvumbuzi wa kihistoria” katika mapango ya jangwani nchini Israel.
Makumi ya vipande vya karatasi vya mabaki hayo viliandikwa kwa Kigiriki, jina la Mungu likionekana kwa Kiebrania.
Machapisho hayo yanayoaminiwa kuwa ya waasi wa kiyahudi waliokimbilia milimani baada ya kuibuka kwa upinzani dhidi ya utawala wa Kirumi katika karne ya pili, yalipatikana wakati wa oparesheni ya kuhifadhi eneo hilo la pangoni lisivamiwe.
Uvumbuzi huo ni wa kwanza kupatikana tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960 wakati mabaki kama hayo na mifupa 40 ilipopatikana katika eneo hilo ambalo limepewa jina pango la ajabu.
Mabaki yaliyopatikana yana machapisho kutoka ya Zakayo na Nahum, ambayo yanajumuisha sehemu ya maandiko yanayojulikana kama kitabu cha Mitume 12 wadogo.