Mabalozi 42 wanaoiwakilisha nchi katika mataifa mbalimbali kesho Agosti 14 watatembelea mradi wa ufuaji umeme wa Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP) uliopo Rufiji Mkoani Pwani kujionea mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa fedha za ndani ili kufanya diplomasia ya kiuchumi katika mataifa wanayotuwakilisha.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na msemaji mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa mabalozi hao wameitwa rasmi kushiriki mikutano ya SADC inayoendelea ambapo Tanzania inakuwa mwenyekiti wa SADC kwa muda wa mwaka mmoja

Mabalozi hao wanaoiwakilisha nchi baada ya kutembelea miradi mbalimbali ukiwepo mradi mkubwa wa kufua umeme wa Julius Nyerere Hydro Power Project  wataenda kutumia vyema kofia zao za ubalozi katika kutangaza vyema diplomasia ya uchumi wa Tanzania katika mataifa mengine hasa yale wanayotuwakilisha.

Amesema kuwa baada ya Prof. Palamagamba Kabudi kupokea uenyekiti wa baraza la mawaziri wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa muda wa mwaka mmoja, kesho Agosti 14, Rais wa kwanza wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini atawasili nchini kwa matukio makubwa mawili.

“Rais Ramaphosa atawasili nchini kesho jioni kwa matukio makubwa mawili kwanza atakuwa na ziara ya kitaifa kwa siku tatu ambapo pia atatembelea kituo cha wapigania uhuru kilichopo Mazimbu Mkoani Morogoro, baada ya kumaliza ziara hiyo tarehe 16 Rais Ramaphosa ataungana na wakuu wa nchi na Serikali katika mkutano mkuu utakaofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu” amesema Dkt. Abbasi

Aidha, amesema kuwa Agosti 15 mwaka huu Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa ataongoza mhadhara wa wazi ambapo ataeleza uzoefu wake juu ya jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kueleza kuwa mhadhara huo ni wa wazi kabisa na kila mmoja anaweza kushiriki ili kuweza kupata uzoefu kutoka kwa mzee Mkapa.

Mkutano huo wa wakuu wa nchi, viongozi wa serikali na wafalme unatarajiwa kuhitimishwa rasmi tarehe 17 na 18 mwaka huu ambapo nchi zote wanachama zimethibitisha kushiriki mkutano huo na wawakilishi wa nchi hizo walianza kushiriki mikutano ya ndani na ile ya wiki ya nne ya viwanda ya SADC.

Bajeti ya Simba msimu huu yawekwa hadharani
Dereva wa Lori lililopinduka apatikana