Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi, wamtetakiwa kuhakikisha wanazitambua na kuziainisha vyema fursa muhimu zilizoko nchini, ili zitumike kusaidia kuinua uchumi wa kimaendeleo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ameyasema hayo mjini Zanzibar wakati akizungumza na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Suleiman Haji Sulemain aliyefika kumuaga akielekea kituo chake cha Kazi Mjini New York nchini Marekani.
Amesema, “Tanzania kama zilivyo nchi zote dunaini inazingatia kutekeleza Diplomasia ya kiuchumi kwa kukaribisha wawekezaji na inaendelea kufunguka kiuchumi kwa kukaribisha ujuzi na mitaji katika ushirikiano ili kuifanya nchi isonge mbele kwa kutumia fursa toka mataifa na Jumuiya mbali mbali Ulimwenguni.”
Aidha, amewataka kufahamu kuwa siasa za dunia kwasasa zimebadilika na hivyo kutumia njia za ziada kuangalia mikakati mbalimbali itakayowezesha kupatokana kwa mitaji na kwamba upo umuhimu wa mabalozi wa Tanzania kuifaidisha nchi kupitia nafasi walizonazo.
Makamu wa Rais, pia amewataka mabalozi kuhakikisha ushiriki wa Tanzania unakuwepo katika masuala mbalimbali muhimu kwa kuwasilisha taarifa za masuala ya nchi zitakazotumika katika kuchangia na kukuza uchumi.
Akiongea ofisini kwa Makamu wa Rais, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Suleiman Haji Suleiman amesema watafuata maelekezo yote kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, zikiwemo Taasisi za Kikanda katika kuunganisha na kutumia fursa tofauti zilizopo duninani.