Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mkakati wa Serikali ni kuimarisha uchumi hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo amewataka mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali kuhakikisha wanatumia uwakilishi wao kutafuta wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini.

Majaliwa amesema hayo leo Februari 7, 2017 alipokutana na mabalozi wa wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Brazil, China, Italy, Ufaransa, Jamuhuri ya Kidemkrasi ya Congo (DRC) na Uswisi, ambapo amewaeleza kuwa jukumu lao ni kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.

Amesema  mkakati wa Serikali ni kuimarisha uchumi  hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo jukumu la mabalozi hao ni kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.

Mabalozi hao ni Balozi Dk. Emmanuel Nchini (Brazil), Balozi Elizabeth Kiondo (Uturuki), Balozi George Madafa (Italy), Balozi James Msekela (Uswisi),Balozi Samuel Shelukindo (Ufaransa), Balozi Paul Meela (DRC), Balozi Mbelwa Kairuki (China).

“Serikali inahitaji watu wa kuja kuwekeza katika viwanda ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza nje ya nchi, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha tunapata wawekezaji wenye sifa,” amesema.

Majaliwa amewataka mabalozi hao kutumia uwakilishi wao katika nchi hizo kwa kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza idadi ya watalii wanaokuja Tanzania.

Aidha, Majaliwa amewataka mabalozi hao kulinda maslahi ya Taifa katika nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na mataifa hayo.

Pia, Majaliwa amewataka mabalozi hao kuhakikisha wanawatambua Watanzania wanaoishi katika mataifa hayo na kushirikiana nao katika kutafuta wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake, Balozi Meela amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watakwenda kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

 

Aubameyang Kumkimbiza Aguero Etihad Stadium
Arsenal FC: Tunasubiri Majibu Ya Vipimo Vya MRI