Mabalozi wateule, wanaokwenda kuwakilisha Tanzania nchi za Zimbabwe, Zambia na Uholanzi, wametakiwa kuitumia vyema Diplomasia ya Kiuchumi kwa kuzitafuta fursa mbalimbali za kibiashara na kuzileta nchini Tanzania.
Wito huo, umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi, Simon Sirro anayekwenda Zambia, Balozi, Luten General Metheu anayekwenda Zimbawe na Balozi, Caroline Chipeta anayekwenda nchini Uholanzi.
Serikali yawageukia Wafanyabiashara wa Mkaa
Amesema, katika nchi wanazokwenda zipo fursa nyingi za kiuchumi na kiutaalamu ambazo zinaaweza kuisaidia Tanzania kujiendeleza zaidi, iwapo mabalozi hao watafanya juhudi ya kuzileta nyumbani ili kusaidia nchi yao.
Othman amewaeleza Mabalozi hao kuwa, Tanzania zipo fursa nyingi za kuchumi za kukuza na kuendeleza sekta ya utalii , biashara na kilimo maeneo ambayo hayajatumika ipasavyo hivyo mabalozi hao wajitahidi kuitumia nafasi hiyo.
Akiongea wakati wa mkutano huo, Kiongozi wa Mabalozi, IGP Mstaafu Simon Sirro amesema maelekezo wanayoyapata kutoka kwa viongozi wakuu ni nyenzo muhimu katika kazi yao na kwamba watajitahidi kuyatumia na kuyafuata ili kuiwakilisha vyema nchi.
Ameongeza kuwa, yeye na wenzake watajitahidi kuhakikisha wanafanya wajibu wao vizuri wa kuitangaza nchi na kushirikiana na watangulizi wao kupitia Diplomasia ya kiuchumi na kukidhi matarajio ya taifa kimaendeleo.