Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ametenga kitita cha milioni mbili kwa ajili ya kununua mabao atakayo funga mshambuliaj wake David Molinga ‘Falcao’ raia wa DR Congo katika Ligi Kuu Bara.
Zahera amesema kwamba atatoa kiasi hicho cha milioni 2,293,230 sawa na dola 1,000 endapo kama itatokea straika wake huyo atashindwa kufunga mabao 15 au zaidi kwenye ligi kuu.
“Mimi ninasema nitatoa kiasi cha dola 1,000 kama itatokea Molinga hatafunga mabao 15 kwenye ligi kuu ninamjua ana uwezo mkubwa wa kufunga tofauti na watu ambavyo wanamchukulia,” alisema Zahera.
“Hapa kwenye kikosi changu tatizo lililopo ni washambuliaji tu kushindwa kufunga mabao. Sisi kwenye mechi moja tunaweza kupata hadi nafasi sita lakini tukafunga mabao machache huku nyingi tukikosa.
“Yaani hatuna shida kabisa kwenye kutengeneza pasi za mabao ila tatizo ni kufunga lakini muda si mrefu nitatengeneza mbinu ambayo itafanya tufunge katika kila nafasi ambayo tunaipata,” alisema Zahera.
Kocha huyo ametenga kitita hiko ikiwa ni baada ya mshambuliaji wake huyo kuanza kuonyesha cheche kwa kufunga mabao matatu kwenye mechi zao mbili zilizopita za kirafiki.
Molinga alifunga mabao hayo kwenye mechi za timu hiyo dhidi ya Pamba SC na Toto African wakati walipokuwa Mwanza wiki chache zilizopita.