Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umesema mwaka huu utaongeza mabasi mengine mapya 95 ikiwa ni sehemu ya hatua za kupunguza msongamano wa abiria kwenye vituo vya mabasi hayo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Dk. Edwin Mhede, alibainisha hayo wakati akifungua mafunzo kuhusu mipango ya mitaa kwa Jiji la Dar es Salaam.
Alisema wakala ulijitahidi kuongeza mabasi 70 hivi karibuni kwa ajili ya kupunguza msongamano huo lakini kutokana na wananchi wengi kuchangamkia usafiri huo, mahitaji yanaendelea kuongezeka.
Alisema zamani abiria alilazimika kusubiri basi kwa dakika 30 lakini walipoongeza mabasi 70, muda huo ulipungua na kufikia dakika tano na kwamba mpango uliopo unalenga kuondoa hata hizo dakika tano ili abiria akifika tu apande basi na kwenda anakotaka.