Wakati Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wakitarajia kuchuana na Al Merrikh keshokutwa Jumamosi (Septemba 30), Kocha Miguel Gamondi, amewataka mabeki wake kuongeza umakini ili kushinda mchezo huo.
Young Africans itacheza na Al Merrikh katika mechi ya marudiano ya hatua ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAFCL), itakayopigwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Timu hiyo itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata katika mchezo wa kwanza uliopigwa katika Uwanja wa Pele, Kigali nchini Rwanda.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Gamondi amesema amekaa na mabeki wake na kuwataka waongeze umakini katika mechi hiyo ili kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Gamondi amesema miongoni mwa maeneo ambayo mabeki wake wamekuwa wakifanya makosa ni wakati wa kuzuia mipira ya kutenga.
“Tunatakiwa kuongeza umakini katika eneo la hatari, mipira ya kutenga sio mizuri, wachezaji wanatakiwa kuwa makini na kuhakikisha haturuhusu mabao katika kila mchezo,” amesema.
Katika mechi sita za mashindano yote msimu huu, Young Africans imeruhusu bao moja pekee hadi sasa.
Bao hilo lilifungwa kwa mkwaju wa Penati na timu ya Asas ya Dijibouti wakati Young Africans ikishinda mabao 5-1, katika mechi ya pili ya hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.