Kocha Mkuu wa Young Africans, Nesreddine Nabi amewapa majukumu mabeki wake na kuwataka kuwa makini ili kuweza kuizuia safu ya ushambuliaji ya Simba SC.
Miamba hiyo ya Soka la Bongo itakutana kesho Jumamosi (Desemba 11), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kocha Nabi amesema kulingana na ugumu wa mchezo huo ana imani utakuwa ya ushindani na safu ya ushambuliaji ya wapinzani wao itaingia kivingine kwa kuhakikisha wanatafuta ushindi dakika za mwazoni.
Amesema wakati kila mchezaji akipewa majukumu yake kuelekea mchezo huo pia amewasisitizia mabeki wake kuwa makini kwa kuwadhibiti washambuliaji wa Simba SC.
“Safu ya ulinzi tayari inajua majukumu yake, washambuliaji nao wanaelewa nini wanatakiwa kufanya katika mchezo huu, ambao utakuwa wa kiufundi na kimbinu zaidi kwa kila upande,” amesema Nabi.
“Tunawaheshimu sana Simba, tunajua ubora na madhaifu yao, tunajiandaa kwa ajili ya kwenda kutafuta pointi muhimu katika mchezo huo,” ameongeza.
Amesema kuhusu kikosi chake hasa kwenye safu ya ulinzi ana imani kila mmoja ana uwezo mkubwa na kufanya vizuri katika mchezo huo kulingana na maandalizi ambayo wanayafanya.