Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amefanya ziara kwenye mradi wa maboresho wa soko la Machinga lililopo Kata ya Iyela Jijini Mbeya, unaotarajia kugharimu kiasi cha Shilingi 540,938,719 milioni.
Akiongea katika ziara hiyo, Malisa amesema eneo hilo limekuwa na changamoto chache hivyo Halmashauri ya Jiji kwa kushirikiana na Serikali Kuu inaendelea kukabiliana na hali hiyo, ili kuhakikisha wafanyabishara wadogo wanafanya shughuli zao katika mazingira rafiki.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa tayari Serikali ya awamu ya sita chini ya Mh.Rais Dkt.Sami Suluhu Hassan imeshatoa zaidi ya shilingi milioni mia tano ili kuhakikisha Machinga wanaondokana na changamoto walizokuwa wanakumbana nazo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dkt. Jonas Lulandala amesema watendaji wao watendaji watasimamia na kuhakikisha miongozo yote iliyotolewa katika kuboresha soko hilo inatekelezwa na kumalizika kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Machinga Jiji la Mbeya, Waziri Hamisi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Shilingi 10 milioni, ili kujenga ofisi ya Shirikisho la Machinga Jiji la Mbeya ambapo ujenzi wa ofisi hiyo unaendelea na amewataka Machinga wanaofanya biashara kwenye maeneo yasiyo rasmi kuondoka kupisha miradi mingine ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa barabara ya njia nne.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Iyela, Mussa Ismaily unakotekelezwa mradi huo amesema hawako tayari kumuangusha Rais Samia, hivyo watahakikisha uwepo wa usalama wa vifaa vya ujenzi na kwamba Wananchi na wadau wa eneo hilo watasimamia ipasavyo ili kusitokee jaribio la ubadhirifu wa mradi.