Klabu za ligi kuu ya soka nchini England (Premier League) zitawasilisha mapendekezo kwenye chama cha soka nchini humo (FA), kuomba dirisha la usajili la nchi hilo lifungwe kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti la National newspapers, klabu za ligi ya England zinajipanga kuwasilisha mapendekezo hayo, kutokana na kushindwa kuvumilia kelele za usajili ambazo zinaendelea kwa sasa ambapo ligi ya nchi hiyo imeshaanza.
Inaaminika kuwa endapo mapendekezo hayo yatakubaliwa na chama cha soka nchini England (FA), mameneja wa klabu za ligi kuu watakua na sababu ya kuwa na utulivu mara baada ya kuanza kwa msimu, tofauti na sasa ambapo baadhi ya mipango yao huvurugwa na ofa zinazotumwa kutoka mataifa mengine kwa ajili ya wachezaji wao muhimu vikosini.
Pendekezo hilo limeambatana na mfano wa purukushani za usajili zinaoendelea kwa sasa dhidi ya kiungo mshambuliaji wa Liverpool, Philippe Coutinho; Ross Barkley wa Everton na kiungo wa Swansea, Gylfi Sigurdsson.
Meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp amewaambia waandishi wa habari nchini Ujerumani kuelekea mchezo wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Hoffenheim kuwa, mapendekezo hayo anaamini yatasaidia kuondoa mkanganyiko ambao kwa sasa umekua mkubwa hususan katika klabu za England.
“Kwa hakika itatusaidia sana sisi mameneja, maana wakati mwingine unashindwa cha kufanya kutokana na ofa ambazo hutumwa kwenye klabu husika. Wakati mwingine zinakuharibia kabisa mipango uliokua umepanga kwa ajili ya msimu wa ligi.” Amesema Klopp.
Mapendekezo hayo yaliafikiwa kwenye kikao kilichowajumisha maeneja wa klabu za ligi kuu ya nchini England kilichofanyika juma lililopita, na wanaamini huenda jambo lao likakubaliwa na kupewa baraka ya kuanza kufanya kazi mwaka ujao.