Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaagiza watendaji wa sekta ya Ardhi katika Halmashauri na Manispaa za Mkoa wa Tabora, kuhakikisha wanarudi katika maeneo wanayoishi wananchi kwa lengo la kutoa elimu kuhusu faida na hasara za kumilikishwa Ardhi.
Hayo yamejiri baada ya Naibu Waziri Mabula kusikitishwa na wamiliki wa Ardhi Mkoa humo waliopimiwa maeneo yao katika zoezi la urasimishaji makazi kushindwa kulipia gharama za upimaji kwa wakati na hivyo kushindwa kumilikishwa maeneo.
Akizungumza leo Agosti 10, 2021 na watendaji wa sekta pamoja na Halmashauri za Mkoa wa Tabora katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwana kiyungi, Dkt Mabula amesema kuwa, serikali inaamua kurasimisha makazi lakini wananchi hawaoneshi mwamko jambo linalokwamisha mipango ya Wizara ya Ardhi katika kumilikisha ardhi wananchi.
Aidha lengo la kuanzishwa zoezi la urasimishaji makazi holela ni kutaka kuwamilikisha wananchi makazi yao sambamba na kuwawezesha kiuchumi.
Naye Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tabora Jabir Singano amemueleza Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa Mkoa wa Tabora umefanya jitihada kubwa ili kukwamua kazi za urasimishaji makazi holela ambapo tangu kuanzishwa ofisi yake idadi ya viwanja vilivyopimwa ni 12,875 na ankara ambazo wamiliki wake wamelipia ni 935 kati ya ankara 3747 zilizotolewa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula yuko mkoani Tabora kwa ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani humo.