Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema serikali inawatambua wamachinga kama kundi maalumu ambalo litasimamiwa na wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii na Makundi maalumu.
Katika Mkutano wake na Viongozi wa wamachinga jijini Dar es Salaam hii leo Januari 25, 20202, Rais Samia amesema katika mipango yote ya serikali vijana wamepewa kipaumbele na wanatakiwa kuonesha mfano.
“Niwapongeze sana kwamba mmejiunda vizuri na sasa serikali inalitambua rasmi kundi hili kwamba ni moja ya makundi maalumu katika yale makundi tuliyoweka kwenye wizara tuliyounda ya maendeleo ya jamii na makundi maalumu, kwa hiyo ni moja ya makundi maalumu yatakayofanya kazi kwa karibu na serikali,” Rais Samia alisema.
Rais Samia amewasisitiza wamachinga wote wawe na vitambulisho maalumu ambavyo vitawasaidia kutambulika katika kila hitaji lao kwa serikali ili kuboresha huduma zote zinazowahusu.
“Kwa sababu ni kundi maalumu, lazima muwe na vitambulisho ambavyo kikiwekwa kwenye mashine kinakuonesha wewe ni nani, sasa hilo tunasubiri tumalize sensa ya watu na makazi,” Rais Samia.
Pia rais Samia amewapa pole na kuwatia moyo wamachinga wote kutokana na majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea katika kipindi kifupi kwa masoko makubwa.
Amesema kuna watu wanafanya hujuma ili kuleta matatizo makubwa ya moto kwa sababu wanakata bima na wanakuwa hawajaona matunda ya bima zao ikiwa ni pamoja na kuchukua mikopo tofauti na kushindwa kuirejesha.
“Mioto hii ina sababu kadhaa huu wa Karume tumeambiwa ni hitilafu ya umeme, lakini lingine ni suala la bima, kuna wale ambao wamekata bima na labda kwa miaka kadhaa hajaona manufaa, anaamua tu ngoja niweke kicheche cha moto hapa kukiungua mimi nitalipwa na bima,” alisema
“Jengine ni hawa wanauchukua mzigo madukani, inawezekana mtu kachukua mzigo mkubwa kauza, moyo wa ushetani unamuingia anaamua asiende kurudisha, anaweka moto kwenye duka atajua tu kuwa moto umewaka Karume au Soko limeungua kwa hiyo sina cha kulipa,” Rais Samia.
Hata hivyo Rais Samia amewapongeza wamachinga wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa watulivu katika wakati wote waliokuwa wakipangwa na halmashauri ya jiji bila kuleta fujo hali iliyosaidia kazi hiyo ikawa na amani na kuisha kwa haraka.
“Natambua kuna watu walikua wanasubiri vurugu zitokee, nchi iharibike, lakini Da res Salaam mmeonesha mfano wakati wa kupangana, mmekua waungwana, mmekuwa wazalendo, mmekwenda kushirikiana na uongozi wa serikali na chama, tulisikia maneno mawili matatu lakini viongozi wa machinga mmetusaidia hali imekuwa shwari pamoja na changamoto zote zilizopo lakini watu wametulia nawashukuru sana,” Rais Samia.
Awali katika hotuba yake ya kumkaribisha Rais, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema kuwa wamachinga walimuomba kila hatua ya ujengaji wa masoko yao washirikishwe.