Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa hotuba muhimu katika ziara yake mjini Kigali nchini Rwanda hii leo ambapo amesema anatambua kwamba nchi yake inabeba jukumu kubwa kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo.

Kiongozi huyo wa Ufaransa amezungumzia kwa kina namna nchi yake ilivyowatelekeza wahanga 800,000 wa mauaji ya kimbari lakini ameepuka kuomba radhi moja kwa moja.

“Wauwaji waliowaandama watu kwenye mabwawa, milimani na makanisani hawakuwa na sura ya Ufaransa,” amesema Macron.

Macron amekuwa Rais wa kwanza wa Ufaransa kuhutubia katika kumbukumbu ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda yaliyotokea mwaka 1994.

“Hawakuwa washirika wa Ufaransa. Damu iliyomwagika haikutokana na silaha zake au mikono ya wanajeshi wake ambao pia walishuhudia kwa macho yao matukio yasiyosemeka,waliwasaidia waliojeruhiwa na kujikaza kutoa machozi, Lakini Ufaransa ina jukumu, ina dhamana ya kihistoria na kisiasa katika nchi ya Rwanda,” amesema Macron.

Rais Paul Kagame ameisifu hotuba ya Macron kwa kutambua jukumu la dhamana iliyobeba Ufaransa katika mauaji hayo ya kimbari ya 1994.

Rais huyo wa Rwanda amesema maneno yaliyotumiwa na Macron yalikuwa na umuhimu mkubwa kuliko kuomba radhi.

Wawili wakamatwa kwa mauaji
Kilio nyumba za ibada katikati ya makazi chamgusa RC Makalla