Wapiga kura nchini Ufaransa jana wamempa ushindi wa muhula wa pili madarakani, Emmanuel Macron katika uchaguzi wa rais baada ya mpinzani wake wa siasa kali za mrengo wa kushoto Marine Le Pen kushindwa kusababisha mshutuko aliotarajia.
Macron alipata asilimia 58.55 ya kura dhidi ya Le Pen aliyepata asilimia 41.45.
Kwa kufanya hivyo, anakuwa kiongozi wa kwanza wa Ufaransa kushinda muhula wa pili katika miongo miwili tangu Jacques Chirac mwaka wa 2002.
Katika hotuba kwa wafuasi wake mbele ya mnara wa Eiffel mjini Paris, Macron alisema atakuwa rais wa kila mtu na kuwa muhula wake wa pili hautakuwa muendelezo wa muhula uliotangulia.
Viongozi kote ulimwenguni wanaendelea kutuma salamu za pongezi. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alikuwa kiongozi wa kwanza kumpongeza Macron kwa simu.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema kwa pamoja watazifanya Ufaransa na Umoja wa Ulaya kusonga mbele.