Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ni lazima rais wa Belarus aondoke madarakani
Akizungumza na gazeti maarufu la kila Jumapili la Journal du Dimanche Macron ameonesha msisitizo wa kuweka shinikizo dhidi ya kiongozi wa muda mrefu wa Belarus, Alexander Lukashenko akisema kwamba lazima Lukashenko aondoke madarakani.
Alhamisi ya wiki iliyopita, Umoja wa Ulaya ulisema kuwa haumtambui Lukashenko kama rais wa Belarus kwa sababu ya maandamano makubwa yanayofanywa na raia wa nchi hiyo wanaotilia shaka matokeo ya kura ya uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita, ambao Lukashenko alitangazwa kushinda kwa kishindo.
Wafuasi wa upinzani na baadhi ya maafisa wa uchaguzi wanadai kuwa mchakato wa uchaguzi ulikumbwa na visa vya udanganyifu.
Katika taarifa kwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ulioandaliwa kwa njia ya video, waziri wa mambo ya nje wa Belarus aliyaonya mataifa ya Magharibi kuingilia ama kuweka vikwazo kuhusiana na uchaguzi huo wa urais ulioibua utata na msako mkali wa serikali dhidi ya waandamanaji.