Bondia Mada Maugo ameibuka na kuwatupia lawama mapromota wa mchezo wa ngumi za kulipwa na kuwaita kama maadui wa mchezo huo ambao kwa kiasi kikubwa umeporomoka kwa hapa nchini.
Maugo ambaye yupo kimya kwa muda mrefu amezungumza na Dar24 na kueleza ya moyoni kuhusu sakata la kutokupanda kwake ulingoni kwa muda mrefu, ambapo amedai kumesababishwa na mapromota ambao hawana dhamira njema na mabondia wa Tanzania.
Alisema ukimya wake umesababishwa na mapromota ambao wameonyesha kushindwa kusimamia misingi ya kazi za mabondia, kwa kutaka kuwalipa ujira mdogo, huku wakitanguliza maslahi yao binafsi.
“Niliamua kukaa pembeni na mchezo wa masumbwi, baada ya kuchoshwa na mapromota uchwara, ambao wameshindwa kuangalia namna ya kuwasiadia mabondia ambao wanahitaji kujikwamua kupitia nguvu na maarifa yao wanapokua ulingoni.
“Mara nyingi nimekua ninawapinga kwa mpango wao wa kutaka kujinufaisha wao binafsi, lakini matokeo yake wananiona kama adui yao, sasa njia rahisi ambayo niliamua kuitumia ni kukaa mbali na mchezo wa masumbwi ili nijishughulishe na mambo mengine.” Alisema Maugo.
Katika hatua nyingine Mada Maugo amelaani mvutano unaoendelea baina ya kamisheni za ngumi za kulipwa ambao umedumu kwa muda mrefu baada ya baraza la michezo la taifa (BMT) kutangaza kuitambua kamisheni ya TPBC.
Amesema mvutano wa kamisheni hizo, umekua kikwazo cha maendeleo ya ngumi za kulipwa hapa nchini na wakati mwingine unaenda mbali zaidi kwa kutaka kuwagawa mabondia.
“Unajua mvutano huu kati ya TPBC dhidi ya TPBO na PST umechangia kushusha mchezo wa ngumi za kulipwa, kila mmoja anahisi ana haki ya kusimamia mchezo huu, lakini ninakuhakikishia hakuna hata mmoja anaweza kufanikiwa katika vita hii, kwa sababu wote hawana sifa za kutambuliwa na serikali (BMT).”
“Hivi juzi aliekua waziri wa habari, utamaduni, Sanaa na Michezo Mh Nape Nnauye alihojiwa katika kipindi cha Dakika 45 cha ITV, alisema wazi kuhusu mvutano huu unaoendelea, yaani alichokisema kimethibitisha ukweli wa usimamizi wa mchezo wa ngumi za kulipwa, yaani mpaka sasa wizara haitambui TPBC wala hizo kamisheni nyingine, kinachoendelea hapa ni utapeli tu.” Alisema Maugo
Wakati huo huo Mada Maugo amethibitisha taarifa za kutarajia kupanda ulingoni kati kati ya mwezi huu dhidi ya mpinzani wake Benson Mwakyembe wa mkoani Ruvuma chini ya Promota Kaike Siraju.
Maugo amesema kwa sasa anajiandaa vyema na mchezo huo ambao utaunguruma mjini Songea siku ya Pasaka na ameahidi kushinda.