Serikali ya Misri imewakamata madaktari ambao wanatuhumiwa kuhusika na mtandao wa biashara ya kuuza viungo vya binadamu.
Jeshi la polisi nchini humo juzi lilivamia katika kituo kimoja maarufu cha afya kinachojihusisha na matibabu ya ini na kuwakamata madaktari kadhaa pamoja na wafanyakazi wengine wa kituo hicho.
Madaktari hao wanatuhumiwa kuondoa viungo vya binadamu kwa wananchi masikini wanaofika katika kituo hicho ikiwa ni pamoja na wakimbizi na kuwauzia wananchi matajiri na watu wa nchi za nje wenye ukwasi mkubwa.
Miaka saba iliyopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitaja Misri kama nchi ya tano kati ya nchi zinazoongoza kwa kufanya biashara ya viungo vya binadamu duniani kote. Taarifa hiyo ilisababisha Serikali ya Misri kuweka sheria kali dhidi ya wanaojihusisha na biashara hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, uchunguzi na oparesheni maalum inayoongozwa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo inalenga hospitali binafsi na vituo vya afya vyenye leseni na visivyokuwa na leseni.