Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imewapokea madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambao wametumwa katika Taasisi hiyo kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nchini.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuwakaribisha madaktari hao iliyofanyika leo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwatuma madaktari hao wa moyo kutoa huduma katika Taasisi hiyo na kuahidi kushirikiana nao kwa muda wote watakaokuwepo hapa nchini.
Prof. Janabi amesema Taasisi hiyo kila baada ya miaka miwili imekuwa ikiwapokea madaktari bingwa wa Moyo kutoka nchini China ambao kwa kiasi kikubwa wamesaidia kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wagonjwa na hivyo kuokoa maisha yao.
“Tumewapokea madaktari watatu ambao ni madaktari bingwa wa wagonjwa ya moyo walioko katika chumba cha uangalizi maalum (ICU), daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo ambao watashirikiana na wataalamu wetu katika kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa”, .
Kwa upande wake kiongozi wa madaktari hao ambaye ni Daktari Bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi Meng Yong ameshukuru kwa mapokezi waliyoyapata na kusema kuwa wamefurahi kuja nchini kutoa huduma kwa watanzania na kuahidi kushirikiana kwa pamoja na wataalamu wa JKCI ili wagonjwa waendelee kupata huduma bora za matibabu.