Jopo la Madaktari jijini London nchini Uingereza limefanikiwa kumuondolea kabisa virusi vya ukimwi muathirika na kumfanya kuwa mtu wa pili duniani kuondolewa virusi hivyo.
Taarifa ya tukio hilo iliyochapishwa kwenye jarida la ‘Nature’ imeeeleza kuwa madaktari hao walifanikiwa kwa kutumia njia ya kupandikiza uboho kutoka kwa mtu ambaye hapokei virusi hivyo (HIV resistant donor).
Kiongozi wa jopo hilo la madaktari, Profesa Ravindra Gupta ambaye ni mtaalamu wa bailojia ya Virusi vya Ukimwi, ameeleza kuwa mgonjwa aliyepewa huduma hiyo ameondolewa virusi vya ukimwi lakini akaonya kuwa ni mapema kusema amepona kabisa.
“Hakuna virusi vya ukimwi ndani yake ambavyo tunaweza kuvipima na kubaini, hatuwezi kubaini chochote… lakini ni mapema kusema kuwa amepona kabisa,” Reuters wanamkariri Profesa Gupta.
Mtu huyo ambaye madaktari wameeleza kuwa ameomba jina lake lisitajwe amekuwa mtu wa pili baada ya Timothy Brown kuondolewa virusi vya ukimwi mwaka 2007, jijini Berlin nchini Ujerumani.
Kama ilivyokuwa kwa Brown aliyebatizwa jina la ‘Berlin Man’ (Mtu wa Berlin), huyu pia amepewa jina la ‘London Man’ (Mtu wa London).
Matibabu pamoja na matokeo ya tiba hiyo yanatarajiwa kuwasilishwa rasmi kwenye mkutano utakaohusu masuala ya tiba, utakaofanyika Jumanne huko Seatle, Washington, Marekani.