Waganga wakuu wa mikoa wameishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, iangalie uwezekano wa kuifanya chanjo ya ugonjwa wa Uviko 19 kuwa ya lazima.
Wito huo wameutoa leo Septemba 17, 2021 Jijini Dodoma wakati katibu Mkuu wa Waganga wa Mikoa na Halmashauri Dkt Japhet Simeo akisoma risala kwenye ufunguzi wa kiakao .
Simeo amesema hayo kufuatia vifo vinavyoendelea kuwakumba baadhi ya wataalamu wa afya walio mstari wa mbele katika kutoa huduma kwa wagonjwa, tangu ugonjwa huo uingie nchini Machi 2020.
Aidha amesema kuwa tangu kuanza kwa janga hilo, nchi imepoteza wataalamu muhimu wa afya waliokuwa mstari wa mbele kuwahudumia wagonjwa wa Uviko-19.
“Kutokana na umuhimu wa chanjo katika kukabiliana na Uviko-19 tunashauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, iangalie uwezekano wa kuifanya chanjo hii kuwa ya lazima kwa watu wote wenye vigezo vya kuchanjwa,” Amesema Simeo.
Dk Simeo ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, ameomba Halmashauri ziwezeshwe kifedha ili ziweze kuwa na ufanisi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.