Madaktari nchini Kenya wamefanikiwa kutoa mswaki kwenye tumbo la mwanaume mmoja aliyeumeza kwa bahati mbaya.
David Charo mwenye umri wa miaka 34, mkaazi wa eneo la Kilifi, ameeleza kuwa alimeza mswaki huo kwa habati mbaya wakati anafanya maandalizi kwenda kazini.
Baada ya tukio hilo, Charo alikimbizwa katika hospitali kuu ya eneo la Pwani na alilazwa akiwa na mswaki huo uliokaa tumboni mwake kwa siku sita.
Alhamisi wiki hii, Charo alieleza kuwa ana hali mbaya na hawezi kupumua kwa sababu anahisi mswaki huo unampa shida zaidi ukiwa tumboni.
Madaktari walifanikiwa kumsaidia Charo, Ijumaa wiki hii. Wanaeleza kuutoa mswaki kwa njia inayojulikana kitaalam kama ‘endoscopy’.
Katibu wa Afya wa Mombasa, Hazel Koitaba, amewaambia waandishi wa habar kuwa afya ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri.
“Kuondolewa kwa mswaki kwenye tumbo la mgonjwa, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika nchini Kenya kwa kutumia njia hii kumefanywa na daktari Ramadhan Omar. Hatua hii imeokoa maisha ya mgonjwa bila kufanyiwa upasuaji wa wazi,” alisema Koitaba.